MWENGE WA UHURU WAZINDUA KITUO CHA POLISI IHANDA-MBOZI, SONGWE
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ally Issu, amesema maendeleo ya kweli hayawezi kufikiwa bila kuwepo kwa amani na usalama wa kudumu, huku akisisitiza kuwa uzinduzi wa Kituo kipya cha Polisi Ihanda ni uthibitisho wa kasi ya maendeleo yanayoendelea kushamiri katika Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.
Akizungumza Oktoba 05, 2025 wakati wa uzinduzi wa kituo hicho chenye hadhi ya Daraja C, Issu alisema kuwa ujenzi wa vituo vya Polisi vya kisasa ni alama muhimu ya maeneo yanayopiga hatua kubwa za kimaendeleo, na kuongeza kuwa uwepo wa kituo hicho ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kiusalama katika eneo hilo.
Aidha, Issu alibainisha kuwa kwa kuzingatia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo, ana imani kuwa Mbozi iko katika mwelekeo sahihi wa kuwa mfano wa maendeleo endelevu katika kanda ya nyanda za juu kusini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamad Rajabu Mbega alisema kuwa Wilaya ya Mbozi inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kutumia mapato ya ndani, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo hicho cha Polisi kata ya Ihanda ili kuimarisha ulinzi na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.
Kituo cha Polisi kata ya Ihanda kimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 140,569,900 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, na kinatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha sheria, amani, na usalama vinadumu katika eneo hilo kwa manufaa ya wananchi wote.



Comments
Post a Comment