NEMC NA ZEMA ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA.


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo, Oktoba 7, 2025, limepokea ugeni wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) na kufanya kikao cha kujengeana uwezo, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kuimarisha ushirikiano katika kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini.


Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema lengo kuu ni kujadiliana mikakati, kutoa ushauri, na kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mazingira ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo na kuongeza tija katika sekta ya mazingira.


Viongozi wa pande zote mbili wamejadili pia utekelezaji wa taratibu walizojiwekea katika kufuatilia na kusimamia sheria za mazingira, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali asilia zinatunzwa ipasavyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZEMA, Bw. Sheha Mjaja Juma, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutimiza wajibu wao kwa kufuata sheria na taratibu za mazingira. Pia amezitaka taasisi za maendeleo kuhakikisha miradi yao inazingatia misingi ya usimamizi endelevu wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.


Itakumbukwa kuwa NEMC na ZEMA wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu, ambapo mara kwa mara wamekuwa wakitembeleana na kubadilishana uzoefu kwa maslahi mapana ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini Tanzania.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.