NIDA YABORESHA USAJILI WA VITAMBULISHO KWA NJIA YA MTANDAO.


Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezindua mfumo mpya wa usajili wa vitambulisho vya Taifa kwa njia ya mtandao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha na kurahisisha huduma za usajili na utambuzi wa watu nchini.


Kupitia mfumo huo wa kidigitali, wananchi wanaweza kujisajili na kutuma maombi yao hatua za awali popote walipo ndani au nje ya nchi bila kulazimika kufika katika ofisi za NIDA za wilaya, hatua inayopunguza foleni na kuokoa muda wa kufuata huduma hiyo ofisini.


Taarifa kutoka NIDA zinaeleza kuwa mfumo huo unamwezesha mwananchi kukamilisha takribani asilimia 75 ya mchakato wa usajili akiwa nyumbani. Hatua inayosalia ni kufika katika ofisi za NIDA wilayani kwa ajili ya uhakiki wa uraia katika dawati la Maafisa Uhamiaji na kuchukuliwa alama za kibaiolojia na Maafisa wa NIDA.


Aidha, mfumo huo umesaidia kuongeza usahihi wa taarifa za waombaji na kupunguza makosa ya kiufundi ambayo hapo awali yalijitokeza kutokana na ujazaji wa fomu kwa mikono.


Wananchi wamesema huduma hiyo imekuwa suluhisho kwa changamoto za muda mrefu za msongamano katika ofisi za usajili, kwani sasa wanaweza kujisajili wakiwa nyumbani au kazini bila usumbufu.


Kwa mujibu wa NIDA, manufaa mengine ya mfumo huo ni pamoja na kuokoa gharama za usafiri, muda wa kufika ofisini mara kwa mara na kuongeza tija kwa wananchi ambao sasa wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji bila usumbufu.


Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi wote kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga Tanzania ya kidigitali, kwa kutumia huduma ya Usajili Kimtandao, ambayo inalenga kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa kwa haraka, ufanisi na kwa usahihi zaidi.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.