NSSC Yawataka Wanasiasa Waache Kuingiza Watoto Katika Shughuli za Kisiasa ili Kulinda Usalama na Haki Zao.


Na Fidea Masunga,Dar es Salaam

Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) umetoa wito kwa wanasiasa nchini kutojihusisha na vitendo vya kuwaingiza watoto katika shughuli za kisiasa, ikiwemo mikutano ya kampeni, maandamano na usafirishaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya siasa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya NSSC, Mratibu wa Shirika la My Legacy, Amina Ally, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Watoto Na.6 ya mwaka 2011 ya Zanzibar, mtoto ni mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18 na haruhusiwi kushiriki kwenye shughuli za kisiasa ama kampeni.


“Sheria zetu ziko wazi. Mtoto hastahili kushiriki kwenye siasa kwa namna yoyote. Wajibu wetu kama jamii ni kuhakikisha anabaki salama, bila kuathiriwa na msukumo wa kisiasa unaoweza kumweka hatarini,” alisema Amina.


Aliongeza kuwa katika kipindi cha chaguzi za nyuma kumekuwapo na matukio ya watoto kuachwa bila uangalizi au kuhusishwa moja kwa moja katika shughuli za kisiasa kinyume cha sheria, hali aliyoeleza kuwa inahatarisha mustakabali wa taifa.


Kwa upande wake, Meneja Utafiti wa Shirika la HakiElimu, Mwemezi Makumba, alisema suala la kulinda haki na usalama wa watoto linapaswa kupewa uzito wa pekee na makundi yote ya kijamii.


“Hili si jukumu la wanasiasa pekee, bali kila mmoja ana nafasi. Vyombo vya habari vina wajibu wa kuelimisha jamii na kuepuka kusambaza ujumbe unaohatarisha watoto, wakati asasi za kiraia zinapaswa kuongeza elimu ya uraia na haki za watoto. Wazazi na walezi nao ni walinzi wa kwanza wa watoto,” alisema Makumba.


Aidha Umoja huo umesisitiza kuwa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuhakikisha maeneo ya mikusanyiko ya umma yanabaki salama na kwamba watoto hawahusishwi kwa namna yoyote na kampeni za kisiasa.


Tamko hilo limetolewa na Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) linaloungananisha mashirika zaidi ya 20 kutoka Tanzania bara na Zanzibar kama sehemu ya harakati zake za kulinda haki za watoto kabla, wakati na baada ya uchaguzimkuu wa mwaka 2025.






Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.