PADRI CAMILLUS NIKATA WA JIMBO KUU LA SONGEA ATOWEKA KIMAAJABU.


Songea.


Jimbo Kuu Katoliki la Songea limethibitisha kutoweka kwa Padri Camillus Nikata, ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) kilichopo Mwanza.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Damian Dallu, Padri Nikata alionekana mara ya mwisho akiwa Songea, alipokuwa amerejea kutoka Dodoma katika mafunzo ya moyo kwa mapadri wanaofundisha katika vyuo vikuu vinavyosimamiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).


Taarifa hiyo inaeleza kuwa Padri Nikata alikaa katika nyumba ya mapadri ya Mtakatifu Vianney Songea, na alikuwa amepanga kusafiri kuelekea Mwanza tarehe 8 Oktoba 2025, kwa basi la SUPERFEO, huku tiketi yake ikiwa imenunuliwa kwa njia ya mtandao.


Hata hivyo, siku ya safari yake, ilibainika kuwa hakuondoka kama ilivyotarajiwa. Mizigo yake aliyokuwa ameandaa kwa safari ilikutwa bado ipo chumbani kwake, na mlango wa chumba ulikuwa umefungwa bila ufunguo kurejeshwa kwa mtumishi wa nyumba hiyo.


“Mtumishi wa nyumba ya mapadri alishangaa kuona mizigo ambayo Padri alitakiwa kuchukua haijachukuliwa, na simu yake haipatikani tangu siku hiyo,” imeelezwa katika taarifa hiyo.


Jimbo la Songea lilijaribu kumtafuta kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuwasiliana na watu aliokaa nao na kwa kutumia simu yake ya mkononi, lakini juhudi hizo hazikufanikiwa. Vilevile, taarifa kutoka ofisi ya kampuni ya usafiri ya SUPERFEO zilibainisha kuwa Padri Nikata alinunua tiketi lakini hakusafiri kwa basi hilo.


Baada ya jitihada zote kushindikana, uongozi wa Jimbo Kuu la Songea umetoa taarifa rasmi kwa Jeshi la Polisi ili kusaidia katika uchunguzi na jitihada za kumtafuta padri huyo.


Askofu Dallu ametoa wito kwa waumini na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama iwapo watakuwa na taarifa zozote zitakazosaidia kupatikana kwake.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.