POLISI: HALI YA USALAMA NI SHWARI, TAARIFA ZA MITANDAONI NI UZUSHI.



Jeshi la Polisi nchini limewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama ni shwari kuelekea siku ya kupiga kura kesho, Oktoba 29, 2025, na kwamba hakuna tishio lolote la kiusalama.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, jeshi hilo limeeleza kuwa maandalizi yote muhimu ya kiusalama yamekamilika na askari wapo tayari kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.


Jeshi hilo limeonya kuhusu kundi la watu wanaoandaa na kusambaza picha na taarifa za matukio ya zamani au ya kutungwa kwa nia ya kupotosha umma na kuleta taharuki. Baadhi ya taarifa hizo zimekuwa zikionekana kwenye mitandao ya kijamii zikiwa na sauti au maandishi yanayoashiria kuwa yametokea hivi karibuni, ilhali si kweli.


Aidha, imeelezwa kuwa wapo watu wanaotengeneza video na picha zenye sura za viongozi na kuzihariri kwa kuziweka sauti na maneno ya kupotosha ili ionekane ni kauli halisi za viongozi hao.


Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa za aina hiyo, vipeperushi na machapisho mengine yanayoenezwa mitandaoni, kwani yamelenga kuleta taharuki na kuvuruga amani ya nchi.


Vilevile, wananchi wamekumbushwa kuwa kusambaza taarifa za uongo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Kimtandao. Badala ya kushiriki kusambaza, wanapaswa kufuta taarifa hizo na kufuatilia taarifa sahihi kutoka kwa mamlaka husika.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.