RC MRINDOKO: HALI YA USALAMA NI SHWARI, WANANCHI WAHIMIZWA KUWAHI VITUONI KUPIGA KURA.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa wakati kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika kesho, tarehe 29 Oktoba 2025.
Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia kituo cha redio cha Mpanda FM, RC Mrindoko ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Katavi kuhakikisha wanawahi mapema katika vituo vyao vya kupigia kura, kwani vituo hivyo vitafunguliwa kuanzia saa moja asubuhi.
Amehimiza wananchi kutekeleza wajibu wao huo kwa amani, utulivu na uzalendo, ili uchaguzi uwe wa mfano wa demokrasia nchini.
"Tunawahimiza wananchi wote wajitokeze mapema siku ya uchaguzi. Ni muhimu tushiriki kwa amani, tukidumisha mshikamano na upendo katika mkoa wetu," amesema RC
Mrindoko.
Amebainisha kuwa maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uchaguzi yamekamilika, na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha zoezi hilo muhimu la kidemokrasia linafanyika kwa utulivu na usalama wa kutosha.
Akizungumzia kata za Katumba na Mishamo, RC Mrindoko amesema kuwa tofauti pekee katika chaguzi wa mwaka huu ni kwamba hakutakuwa na upigaji kura ndani ya maeneo hayo, kwa kuwa yametambuliwa kama kambi za wakimbizi kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi inayoongozwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa wananchi wote waliojiandikisha watapiga kura kama kawaida lakini nje ya maeneo hayo katika vituo vilivyoidhinishwa.
Aidha, RC Mrindoko ameihakikishia jamii kuwa hali ya usalama katika Mkoa wa Katavi ni shwari, na serikali ya mkoa inaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wote wanashiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.

Comments
Post a Comment