SERIKALI YATANGAZA KIMA KIPYA CHA CHINI CHA MSHAHARA SEKTA BINAFSI; KITAKACHOANZA KUTUMIKA JANUARI MOSI, 2026.



Na Fidea Masunga,DAR ES SALAAM.


 Serikali imetangaza kima cha chini cha mshahara kipya kwa sekta binafsi, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wafanyakazi, kuhakikisha malipo ya haki, na kuimarisha tija katika sekta binafsi. 


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alisema mchakato huo wa upangaji wa kima kipya cha mshahara umekamilika ambapo Amri mpya ya Kima cha Chini cha Mshahara imechapishwa rasmi katika Gazeti la Serikali Namba 605A la tarehe 13 Oktoba 2025.


Alisema Sekta zenye kima cha chini cha mshahara zimeongezeka kutoka 13 mwaka 2022 hadi 16 mwaka 2025, huku sekta ndogo zikiongezeka kutoka 25 hadi 46 huku kima cha chini cha mshahara kwa wastani kimeongezeka kwa asilimia 33.4, kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/=.


Aidha Ongezeko hilo linagusa sekta nyingi, ikiwemo kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi, michezo, utamaduni na huduma nyinginezo. Kima kipya cha mshahara kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026.


Waziri Kikwete alisisitiza kuwa ongezeko hilo limezingatia vigezo vya msingi, ikiwa ni pamoja na uwezo wa waajiri kulipa mshahara mpya, ongezeko la gharama za maisha, tija ya biashara, na dira ya taifa katika kukuza uchumi, ajira, na kazi zenye staha. 


Alisisitiza kuwa waajiri wote wa sekta binafsi lazima watekeleze amri hii, kwani ni takwa la kisheria. Ofisi yake itaendelea kufuatilia utekelezaji, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi, na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha sheria hii inatekelezwa kikamilifu.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Rehema Ludanga, alisema:

“Ongezeko hili ni fursa muhimu kwa wafanyakazi wa sekta binafsi. Tunawaasa wafanyakazi kuwa na uelewa wa haki zao, na pia kuhimiza waajiri kutumia ongezeko hili kikamilifu kwa manufaa ya wote. TUCTA itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha utekelezaji wa amri hii unafanyika ipasavyo.”



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.