TAMWA na GIZ waendesha warsha ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Na Fidea Masunga,Dar es Salaam
Chama cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kimeendesha warsha ya majadiliano maalum kupitia mradi wa Sauti Zetu yenye lengo la kutathmini hali ya ukatili wa kijinsia na kutafuta mbinu za kudumu za kuumaliza tatizo hilo nchini.
Warsha hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo walimu, viongozi wa dini, wanafunzi pamoja na wanaharakati wa kijamii.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, alisema aina ya ukatili wa kijinsia unaoacha madhara makubwa zaidi kwa wahanga ni ule wa kisaikolojia kwa kuwa huathiri moja kwa moja afya ya akili na maisha ya kila siku ya mwathirika.
“Ukatili wa kisaikolojia mara nyingi hauonekani kwa macho kama ilivyo kwa ukatili wa kimwili, lakini madhara yake ni makubwa zaidi na huathiri familia nzima. Tunahitaji jamii na viongozi wa dini kushirikiana kikamilifu ili kupata suluhu ya kudumu ya kuumaliza ukatili huu,” alisema Dkt. Reuben
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa warsha hiyo ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mugabe, aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa karibu zaidi na watoto wao, ili kuwakinga dhidi ya changamoto zinazotokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Mtoto anapokuwa karibu na mzazi wake, anapata nafasi ya kueleza changamoto anazokabiliana nazo, jambo linalosaidia kuzuia ukatili mapema kabla haujawa mkubwa,” alisema.
Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Sauti Zetu unaolenga kuimarisha sauti za wanawake na vijana katika kupinga ukatili wa kijinsia na kuchochea mshikamano wa jamii katika mapambano hayo.






Comments
Post a Comment