TMA Yatabiri Mvua Chache Msimu wa Novemba 2025–Aprili 2026, Wakulima na Wafugaji Watahadharishwa.


Na Fidea Masunga,Dar es salaam.

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026, ikibainisha kuwa maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua chache zenye kiwango cha wastani hadi chini ya wastani.


Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza mwelekeo huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, alisema hali hiyo inaweza kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hasa kilimo, mifugo, na upatikanaji wa maji.


“Kwa msimu huu, tunatarajia upungufu wa unyevunyevu ardhini, kupungua kwa kina cha maji katika vyanzo vya maji vinavyotumika na jamii, upungufu wa malisho kwa mifugo na wanyamapori, pamoja na changamoto katika sekta ya usafirishaji,” alisema Dk. Chang’a.


Kwa mujibu wa TMA, mvua za msimu zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu hadi ya nne ya Oktoba katika ukanda wa Magharibi unaojumuisha mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida, na kuendelea taratibu katika maeneo mengine ya nchi.


Kwa Kanda ya Kati (mikoa ya Dodoma na Singida), mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya Desemba na kuisha wiki ya tatu hadi ya nne ya Aprili 2026, zikiwa chini ya wastani hadi wastani.


Aidha, kwa Nyanda za Juu Kusini Magharibi (mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Iringa), mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi ya tatu ya Novemba na kuisha mwishoni mwa Aprili hadi mapema Mei, zikiwa pia katika kiwango cha chini ya wastani hadi wastani.


TMA imetoa wito kwa wakulima, wafugaji, na wadau wengine wa maendeleo kuchukua tahadhari na kutumia taarifa za utabiri kwa kupanga shughuli zao kwa ufanisi, ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa mvua msimu huu.





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.