TMA YATAHADHARISHA WANANCHI KUHUSU KIMBUNGA “CHENGE”; MAENEO YA PWANI YAPEWAA ANGALIZO.

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya pwani, kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kufuatia kuwepo kwa kimbunga “Chenge” kilichopo katika Bahari ya Hindi, kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar.


Kimbunga hicho kimeendelea kusalia baharini kikisogea magharibi, huku kikionesha kupungua kwa kasi na nguvu zake kadri kinavyosogea. Hadi asubuhi ya leo, kilikuwa umbali wa takribani kilometa 1,280 mashariki mwa pwani ya Kisiwa cha Mafia.


Tathmini ya mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinaweza kusababisha ongezeko la upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Oktoba 26 hadi 28, mwaka huu.


Maeneo yanayotarajiwa kuathirika zaidi ni visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga. Hata hivyo, kimbunga hicho hakitarajiwi kuingia moja kwa moja nchini, ila athari ndogo kama vipindi vya mvua kubwa na mawimbi makubwa vinaweza kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya pwani.


Kutokana na hali hiyo, TMA imehimiza wavuvi, watumiaji wa vyombo vya baharini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuwa makini na kufuatilia taarifa rasmi za utabiri wa hali ya hewa ili kupata tahadhari na ushauri wa kitaalamu kwa wakati.


Mamlaka hiyo pia imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa Kimbunga “Chenge” na kutoa taarifa zaidi kadri hali itakavyoendelea kubadilika katika Bahari ya Hindi.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.