WAHITIMU 680 WA JESHI LA UHIFADHI WATUNUKIWA VYETI, DKT. ABBASI AWATAKA KUWA WAZALENDO.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amefunga rasmi mafunzo ya nadharia na vitendo ya viongozi kwa Maafisa na Askari 311 wa Jeshi la Uhifadhi kutoka TANAPA, pamoja na mafunzo ya awali ya Askari 369 wa TFS, yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo cha Jeshi la Uhifadhi Mlele, mkoani Katavi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Abbasi aliwataka wahitimu kutekeleza mafunzo waliyopata kwa vitendo, kufanya kazi kwa ushirikiano, na kuongeza uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda rasilimali za Taifa.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana kupitia sekta ya Maliasili na Utalii, pamoja na sekta nyingine nchini.
Pia alieleza kuwa kibali cha kuajiri askari 311 na wengine zaidi ya 500 wanaotarajiwa kujiunga na mafunzo hayo ni kielelezo cha dhamira ya serikali kuimarisha Jeshi la Uhifadhi na kuboresha maisha ya vijana.
Dkt. Abbasi aliwahimiza wahitimu hao kuwa mfano wa nidhamu, uadilifu na uwajibikaji kazini, akisisitiza umuhimu wa kutumia maarifa na mbinu walizopata kuleta tija katika uhifadhi wa misitu, wanyamapori na rasilimali nyingine za taifa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo, aliwapongeza wahitimu kwa kukamilisha mafunzo yao na kuwataka kutumia ujuzi huo kuendeleza sekta ya uhifadhi na utalii, akisisitiza umuhimu wa kulinda misitu na rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mafunzo hayo yamekuwa sehemu ya jitihada za serikali za kuimarisha Jeshi la Uhifadhi, kuongeza ufanisi katika uhifadhi wa maliasili, na kuendelea kutoa fursa za ajira kwa vijana nchini.



Comments
Post a Comment