NIDA YAWAHAIMIZA WANANCHI KUTUMIA VYANZO RASMI VYA MAWASILIANO KUEPUKA MATAPELI.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewahimiza wananchi kote nchini kutumia vyanzo rasmi vya mawasiliano wanapohitaji huduma za usajili na utambuzi wa watu, ili kuepuka kutapeliwa na watu wasio waaminifu wanaojifanya maafisa wa mamlaka hiyo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa wimbi la matapeli wanaotuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kwa wananchi, wakiwataka kutuma fedha kwenye namba za simu za mkononi ili wapatiwe huduma za usajili au marekebisho ya taarifa kwa haraka.
NIDA imeeleza kuwa malipo yote ya huduma za Serikali hufanyika kupitia mfumo rasmi wa Huduma za Serikali (Control Number) na si kwa namba za simu za mkononi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia taratibu rasmi.
“Malipo yoyote yanayohusiana na huduma za Serikali hufanyika kupitia Control Number na si kwa namba za simu. Tunawaomba wananchi wawe makini na taarifa za uongo zinazosambazwa na matapeli,” imeeleza Mamlaka hiyo.
Aidha, NIDA imewataka wananchi wanaopokea ujumbe wa aina hiyo kutoa taarifa mara moja katika vyombo vya usalama kama Polisi au TAKUKURU, au kupitia vyanzo rasmi vya mawasiliano vya mamlaka hiyo ambavyo ni,Kituo cha Huduma kwa Wateja: 0232 210 500,Barua pepe: info@nida.go.tz,Tovuti: www.nida.go.tz na Ofisi za Usajili za NIDA katika kila wilaya nchini.
Mbali na njia hizo, wananchi wanaweza pia kuripoti matapeli kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) kupitia mfumo wa SIVIS kwa kutuma ujumbe kwenda namba 15040, kisha kuandika neno TAPELI na kufuata maelekezo yatakayotolewa.
Kwa mujibu wa NIDA, taarifa hizo zitafanyiwa ufuatiliaji wa haraka na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo vya udanganyifu.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha matapeli wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu wanachukuliwa hatua kali, huku ikiendelea kuboresha mifumo ya mawasiliano na utoaji huduma kwa wananchi.

Comments
Post a Comment