WATANZANIA WAMETAKIWA KULINDA AMANI KABLA NA BAADA YA UCHAGUZI.

Na Fidea Masunga, Kibaha

Wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Watanzania wametakiwa kuendelea kudumisha na kuilinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na utulivu na mshikamano wa kitaifa.


Wito huo umetolewa na Mchungaji John Makomele ambae ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Baptist lililopo Lulanzi, Kibaha mkoani Pwani, wakati wa maadhimisho ya miaka tisa (9) tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mchungaji  Makomele alisema ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anachangia katika kudumisha amani kwa maneno, matendo na mwenendo unaoleta umoja, hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu.


“Uchaguzi ni tukio la kidemokrasia linalopaswa kuleta umoja na siyo chuki. Tuwaheshimu viongozi wetu, tuombe kwa ajili ya taifa, na tuwe walinzi wa amani,” alisema Mchungaji Makomele.


Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri upendo, uadilifu na mshikamano ili kusaidia jamii kuwa na mwelekeo chanya katika kipindi hiki nyeti kwa taifa.


Kanisa la Baptist Lulanzi lilianzishwa mwezi Oktoba mwaka 2016 chini ya uongozi wa Mchungaji John Makomele, likianza shughuli zake za ibada chini ya mti kabla ya kujenga jengo la ibada lililopo sasa. 


Hata hivyo Maadhimisho hayo ya miaka tisa ya Kanisa la Baptist yalihudhuriwa na waumini wa kanisa hilo, wageni waalikwa pamoja na viongozi wa dini mbalimbali, ambapo walitumia fursa hiyo kumshukuru Mungu kwa hatua iliyofikiwa na kuombea taifa liendelee kuwa na amani na umoja.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.