WATUMISHI WA UMMA WAASWA KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29.
Na Fidea Masunga, Dar es Salaam.
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imewataka watumishi wote wa umma waliopo katika taasisi na mashirika ya umma nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kaimu Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, alisema kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kiraia unaojenga demokrasia, umoja na uthabiti wa Taifa.
“Watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano kwa jamii kwa kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura. Kupiga kura ni chombo cha mabadiliko chanya kinachowawezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu na uwajibikaji,” alisema Bi. Mauki.
Aliongeza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi.
Kwa mujibu wa Bi. Mauki, ofisi hiyo inatambua umuhimu wa rasilimali watu katika taasisi za umma, hivyo imewataka wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha watumishi wanapatiwa fursa ya kushiriki uchaguzi bila kuathiri majukumu yao ya kazi.
“Tunatoa wito kwa watumishi wote wa umma kutumia haki yao ya kupiga kura kwa amani, kwa kufuata sheria na taratibu za nchi. Ushiriki wao ni alama ya uwajibikaji, uzalendo na dhamira ya kweli ya kuimarisha utawala bora,” aliongeza.
Bi. Mauki alisema OMH itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma katika kuhakikisha kunakuwepo usimamizi bora wa rasilimali watu na kuimarisha mchango wa sekta ya umma katika kukuza uchumi wa Taifa.

Comments
Post a Comment