DALALI WA MAHAKAMA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA WIZI WA KUAMINIWA MKOANI GEITA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia Wema Haibe (38), dalali wa Mahakama, kwa tuhuma za wizi wa kuaminiwa baada ya kudaiwa kuuza nyumba aliyokabidhiwa na Mahakama kisha kufuja fedha zaidi ya Shilingi milioni 22.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Polisi, mtuhumiwa alikuwa na dhamana ya kutekeleza amri ya Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Geita Kituo cha Nyankumbu, kufuatia shauri la talaka namba 65/2024.
Mahakama ilielekeza nyumba ya wanandoa Joseph Kalinda na Ndimira Kasisi, iliyopo katika eneo la Fadhili Bucha, Kata ya Buhalahala, Wilayani Geita, iuzwe kwa mnada na fedha zote ziwekwe kwenye akaunti ya Mahakama kama taratibu zinavyoelekeza.
Hata hivyo, mnamo Aprili 4, 2025, Wema Haibe anadaiwa kuiuza nyumba hiyo kwa Tatizo Balanzila (56) kwa Shilingi milioni 22, lakini badala ya kuziwasilisha fedha hizo kwenye akaunti ya Mahakama, aliziingiza kwenye akaunti binafsi kinyume na maelekezo ya kisheria.
Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa awali unaendelea na mara baada ya hatua za awali kukamilika, mtuhumiwa atasafilishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Polisi imetoa onyo kwa madalali wa Mahakama na watu wote wanaotekeleza amri mbalimbali za Mahakama kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na kufuata taratibu zote za kisheria, ili kuepusha vitendo vya wizi na matumizi mabaya ya madaraka.

Comments
Post a Comment