DC Ilala Aipongeza GSM Foundation, Amana kwa Kutoa Huduma za Ubingwa Bobezi Bure
Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, ameipongeza Taasisi ya GSM Foundation pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana kwa kuendesha kambi ya uchunguzi na matibabu ya ubingwa bobezi bila malipo, sambamba na kugawa bima za afya kwa wananchi 300 wakiwemo wanawake, watoto na wazee wasio na uwezo.
Mhe. Mpogolo alitoa pongezi hizo alipotembelea kambi hiyo kwa lengo la kukagua hali ya utoaji wa huduma na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na huduma ambazo zimesogezwa karibu yao, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhimiza Bima ya Afya kwa Wote na kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Amesema kuwa huduma zinazotolewa na madaktari bingwa katika kambi hiyo ni za ubingwa bobezi ambazo kwa kawaida hupatikana kwa gharama kubwa, hivyo kutoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kujitokeza mapema ili kuchangamkia fursa hiyo muhimu inayogusa rika zote.
“Nawapongeza GSM Foundation na Hospitali ya Amana kwa kutuletea huduma hizi za kibingwa. Kambi hii imekuwa ya kipekee kwani kila mwananchi atakayebainika kuwa na changamoto za kiafya ataandikiwa rufaa na kulipiwa gharama za matibabu na GSM Foundation,” alisema Mhe. Mpogolo.
Baadhi ya wananchi waliopata huduma kupitia kambi hiyo wamesema wamehudumiwa kwa haraka bila gharama zozote, huku wakitoa wito kwa wengine kujitokeza ili kunufaika na huduma hizo za bure.

Comments
Post a Comment