DK MWIGULU NCHEMBA AAPISHWA RASMI KUWA WAZIRI MKUU WA TANZANIA.
Baada ya uteuzi na kuidhinishwa na Bunge, hatimaye Dk Mwigulu Nchemba ameapishwa rasmi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge huyo wa Iramba Mashariki ameapishwa leo Ijumaa, Novemba 14, 2025, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kuapishwa kwake kunafungua ukurasa mpya wa utekelezaji wa majukumu ya mtendaji mkuu wa Serikali ya Awamu ya Sita, katika kipindi cha pili cha uongozi wa Rais Samia.
Dk Mwigulu ameteuliwa kushika nafasi hiyo akichukua nafasi ya Kassim Majaliwa, ambaye amehudumu kama Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2015 chini ya Serikali ya Hayati Dkt. John Magufuli.
Mara baada ya kuapishwa, Dk Mwigulu ameahidi kushirikiana na watendaji wote wa Serikali kusukuma mbele ajenda za maendeleo, kusimamia nidhamu ya matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika sekta zote.
Rais Samia, akizungumza katika hafla hiyo, amempongeza Waziri Mkuu huyo mpya na kumtaka aendeleze misingi ya uwajibikaji, uadilifu, uwazi na utendaji wa kazi kwa matokeo, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kujenga mifumo madhubuti ya kuhimiza maendeleo na ustawi wa Watanzania.



Comments
Post a Comment