DKT. KIJAJI AITAKA JAMII KUJIFUNZA HISTORIA YA TAZARA.


Na Fidea Masunga, Dar es Salaam.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesisitiza umuhimu wa jamii kujifunza Historia ya Reli ya Tanzania–Zambia (TAZARA) ili kuimarisha uelewa wa urithi wa taifa na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Akizungumza katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa onesho maalum la Historia ya TAZARA, lililofanyika katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam, Dkt. Kijaji alieleza kuwa onesho hilo litadumu kwa miezi miwili likiwa limelenga kutoa elimu endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu nafasi ya reli hiyo katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na juhudi za ukombozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika.


Amebainisha kuwa TAZARA, iliyojengwa mwaka 1970 kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Serikali ya China, ni mfano muhimu wa mafanikio ya miundombinu barani Afrika na ishara ya kudumu ya ushirikiano wa kihistoria kati ya Afrika na China ambapo reli hiyo imekua ikichangia katika usafirishaji wa watu na bidhaa hali inayochochea kuimarisha shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania, Zambia na masoko jirani.


“TAZARA ni urithi wa kimkakati tuliorithishwa na waasisi wetu. Ni wajibu wetu kuuhifadhi, kuutunza na kuuendeleza chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhifadhi wa Urithi wetu,” alisema Dkt. Kijaji.


Aidha, aliwataka wananchi kutembelea onesho hilo kwa wingi, akisisitiza kuwa uelewa wa historia ya taifa ni msingi muhimu wa kujenga utambulisho wa kitaifa, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kudumisha tunu za amani na utu.


Kwa upande wake Balozi wa China Tanzania,Mhe. Chen Mingjian, alifafanua kuwa TAZARA ni mfano wa mshikamano wa kihistoria kati ya China na nchi za Afrika, na kuonyesha thamani ya ushirikiano wa kimaendeleo unaolenga kuleta manufaa kwa wananchi. Alisisitiza kuwa China inaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhifadhi, kuendeleza na kutunza urithi huu muhimu.


Hafla hiyo iliambatana na Onesho lililowasilisha machapisho, michoro na mikusanyo ya kihistoria huku likiambatana na burudani za ngoma za asili kwa madhumuni ya kukuza uelewa na kuvutia washiriki wa rika mbalimbali.






Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.