DKT. MWIGULU AZUNGUMZA NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI.
Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amezungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Novemba 25, 2025, ambapo amesisitiza kuwa Tanzania na rasilimali zake zitalindwa kwa gharama yoyote ile.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kuwa makini na makundi yenye nia ya kuichafua na kuiharibu nchi, akisema kuwa Tanzania ni nchi nzuri inayopaswa kulindwa dhidi ya watu wenye malengo mabaya.
Amesema kuwa baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa wanatamani mabaya yaendelee kutokea, hivyo Watanzania wanapaswa kuwakataa na kutokubali kutumiwa kufanya uovu dhidi ya nchi.
“Kila mmoja alibebe jambo hili kwa uzito. Hawatupendi; wanaangalia rasilimali zetu. Nchi yetu si masikini, wapo wanaomezea mate rasilimali zetu. Ninawahakikishia tutailinda Tanzania na rasilimali zake kwa gharama yoyote ile,” amesema Dkt. Mwigulu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuwa na dhamira ya dhati na kuunganisha nguvu katika kuilinda na kuitunza nchi, akiwataka viongozi wa serikali katika ngazi zote kuwa makini na kila anayeingia katika maeneo yao.
Akiendelea, Dkt. Mwigulu amesema kuwa hatutaweza kupambana na umasikini endapo tutawachukulia wawekezaji au sekta binafsi kama maadui.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya mabadiliko ya sheria yanayowezesha wakandarasi wa ndani kupata miradi mikubwa, huku wakandarasi wakubwa wakitakiwa kuomba zabuni ndogo (subcontracts) kwaohatua ambayo itafungua fursa zaidi kwa vijana wa Kitanzania.


Comments
Post a Comment