KIKWETE APONGEZA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA KWA KUIMARISHA UTENDAJI NA UFANISI KATIKA SEKTA YA UTUMISHI WA UMMA.
Na Fidea Masunga,Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, amekipongeza Chuo cha Utumishi wa Umma kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha utendaji, uwazi na ufanisi wa watumishi wa umma nchini.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es salaam katika makao makuu ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania,wakati akizungumza na Menejimenti ya chuo hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kujionea utekelezaji wa majukumu ya chuo.
Mhe. Kikwete amesema kuwa chuo kina nafasi muhimu katika kutoa mwongozo wa kistratejia na kitaaluma kwa utumishi wa umma, hususan katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 huku akisisitiza chuo kuendeleza tafiti na mafunzo ya vitendo yanayolenga kuboresha ujuzi, utendaji na uzalishaji wa watumishi wa umma.
Pia,Mhe. Kikwete ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na chuo ili kuhakikisha kinaendelea kutimiza majukumu yake kikamilifu na kuchangia moja kwa moja katika kuboresha maadili na huduma za utumishi wa umma nchini.
Awali, Akitoa taarifa ya utendaji wa chuo kwa kipindi cha miaka minne (2021/22 – 2024/25), Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo wa Utumishi wa Umma,Dkt. Ernest Mabonesho, amesema chuo kimefanikiwa kutoa mafunzo kwa watumishi 46,964, sawa na wastani wa watumishi 11,741 kwa mwaka, huku kikiendesha mafunzo kwa jumla ya wanachuo 43,753 katika ngazi za Shahada, Stashahada na Astashahada katika fani mbalimbali za Menejimenti ya Kumbukumbu, Nyaraka na Taarifa, Uhazili na Utawala, Rasilimali Watu, na Ununuzi na Ugavi.



Comments
Post a Comment