MADAKTARI TARAJALI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA AMANA WATAKIWA KUJITUMA NA KUZINGATIA MAADILI YA TAALUMA YAO.
Madaktari tarajali wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana wametakiwa kujituma na kufanya kazi kwa weledi, wakizingatia Sheria, Kanuni, na Maadili ya taaluma yao ili kufanikisha azma ya hospitali hiyo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Jumanne Mafele, wakati akifungua mafunzo elekezi kwa madaktari tarajali 36 wanaoanza rasmi kipindi cha mafunzo yao hospitalini hapo.
Dkt. Mafele alisema kuwa Hospitali ya Amana ni miongoni mwa hospitali za rufaa zinazoongoza kwa utoaji wa huduma bora, hivyo ujio wa madaktari hao utakuwa chachu katika kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
“Kuwa daktari si kazi tu, ni wito wa moyo na uaminifu mkubwa. Nawasisitiza mfanye kazi kwa uaminifu, mtunze siri za wagonjwa na mtumie lugha ya upendo kwa wateja,” alisema Dkt. Mafele.
Aidha, aliwahimiza madaktari hao kutumia fursa hiyo kujifunza kwa vitendo kutoka kwa wataalamu waliobobea katika sekta ya afya, akibainisha kuwa uzoefu huo utawajenga kitaaluma na kuwasaidia kutoa huduma bora zaidi.
Kwa upande wao, madaktari tarajali hao walishukuru uongozi wa hospitali kwa kuandaa mafunzo hayo, wakiahidi kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kuzingatia maadili ya taaluma ya udaktari katika kipindi chote cha mafunzo yao.

Comments
Post a Comment