MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA YATOA MWENENDO NA MATARAJIO YA MVUA KWA SIKU 10 KUANZIA NOVEMBA 21, 2025.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA imetabiri kurejea kwa mvua katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia Novemba 21 hadi 30 2025 huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kuendelea kuwa na hali ya ukavu.
Kwa mujibu wa TMA, mabadiliko ya mifumo ya hewa duniani yanachangia kusogea kwa ukanda wa mvua ITCZ kuelekea kusini hatua inayosababisha maeneo ya Ziwa Victoria, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini Magharibi na baadhi ya mikoa ya pwani kuanza kupata mvua za vipindi huku upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini ukiendelea kuimarika na kuleta hali ya mawingu katika ukanda wa pwani.
Katika Kanda ya Ziwa Victoria, wakazi wa Mwanza, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara wanatarajia kuona mvua za vipindi zilizoambatana na ngurumo hasa mwanzoni mwa kipindi Hali kama hiyo inatazamiwa kujitokeza pia Kigoma, Katavi na Tabora.
Kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini Magharibi, mvua zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo kadhaa huku Ruvuma na kusini mwa Morogoro zikipata mvua nyepesi Dodoma na Singida pia zinatarajiwa kuanza kupata mvua mwanzoni mwa dekadi hii jambo linaloweza kuleta nafuu kwa wakulima wanaoanza maandalizi ya mashamba.
Pwani ya Kusini hususan Lindi na Mtwara inatarajiwa kupata mvua za vipindi wakati Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba vikitazamiwa kupata mvua hasa mwanzoni mwa kipindi kutokana na upepo wa baharini kushika kasi.
Hata hivyo, mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara inatarajiwa kuendelea kuwa na ukavu kwa sababu mifumo ya hewa haijatosha kuleta mvua kwa wakati huu.
TMA imewataka wananchi kufuatilia taarifa zake ili waweze kupanga shughuli za kila siku hasa sekta zinazotegemea mvua kama kilimo, uvuvi na usafiri.

Comments
Post a Comment