Mwigulu Afanya Ziara ya Kushtukiza, Aitaka Sekta ya Afya Kuboresha Huduma kwa Wajawazito.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Novemba 15, 2025 amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuagiza hospitali zote nchini kuhakikisha wajawazito wanahudumiwa haraka ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma kwa wajawazito na kuhakikisha hakuna ucheleweshaji unaoweza kuhatarisha afya ya mama au mtoto.
Amezielekeza Wizara ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na hospitali zote nchini kuhakikisha zinakuwa na dawa za kutosha kulingana na mahitaji ya maeneo yao. Alibainisha kuwa wananchi hawapaswi kufanyiwa vipimo hospitalini kisha kuambiwa wanunue dawa nje, akitaka hospitali za serikali ziwe na uwezo wa kutoa huduma kamili.
Aidha, Waziri Mkuu amezikumbusha hospitali kuweka vifaa muhimu vya usafi katika wodi za wazazi, ikiwa ni pamoja na ndoo na mabeseni, ili kuwasaidia akinamama wanaowasili bila vifaa hivyo. Alieleza kuwa vifaa hivyo ni vya msingi na hospitali zinapaswa kuwa navyo muda wote.
Dkt. Mwigulu ametumia ziara hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na miundombinu ya kutolea huduma.
Wakati wa ziara hiyo, wananchi na wagonjwa waliomweleza Waziri Mkuu wamethibitisha kuwa huduma katika hospitali hiyo zinatolewa kwa uangalizi na kwa kuzingatia mahitaji ya wagonjwa.
Comments
Post a Comment