PROF. SHEMDOE ATOA SIKU NNE HUDUMA YA MWENDOKASI KUREJEA KATIKA MAENEO YOTE YA JIJI LA DAR ES SALAAM.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameagiza kurejeshwa kikamilifu kwa huduma ya mabasi ya mwendokasi (DART) katika maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam ndani ya kipindi cha siku nne kuanzia leo.
Prof. Shemdoe alitoa maelekezo hayo Novemba 29, 2025 wakati wa uzinduzi wa safari za mabasi ya mwendokasi kutoka Kituo cha Ubungo Maji kwenda Gerezani, safari ambayo imeanza upya baada ya kusimama tangu Oktoba 29, 2025 kufuatia vurugu zilizosababisha uharibifu wa baadhi ya miundombinu ikiwemo vituo vya mabasi katika maeneo kadhaa ya jiji.
Akizungumza katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe alisema kurejea kwa huduma hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, aliyetoa muda wa siku 10 kuhakikisha usafiri huo muhimu unarejea kwa wananchi. Hata hivyo, Prof. Shemdoe alibainisha kuwa utekelezaji huo umefanyika kwa kasi zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
“Mhe. Waziri Mkuu alituelekeza ndani ya siku 10 tuwe tumekamilisha marekebisho ya muda kutoka hapa Gerezani hadi Kimara. Leo nina furaha kusema kwamba ndani ya siku sita tumeweza kusogeza huduma hii hadi Ubungo Maji,” amesema Prof. Shemdoe.
Ameongeza kuwa juhudi za ukarabati wa miundombinu iliyoharibika katika maeneo ya Kimara, Magomeni na Morocco zinaendelea kwa kasi kwa ushirikiano wa pamoja kati ya DART, UDART, TANESCO na TANROADS. Alisisitiza kuwa hakuna sababu yoyote itakayozuia huduma hizo kurejea kikamilifu ndani ya siku nne kama alivyoelekeza.
Prof. Shemdoe ameahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam wanaendelea kupata huduma ya usafiri wa uhakika, salama na wa uhakika kupitia mfumo wa mwendokasi, ambao ni uti wa mgongo wa usafiri wa umma jijini.

Comments
Post a Comment