Rais Mwinyi Awaapisha Mawaziri, Aamuru Kasi Mpya ya Utekelezaji na Kuwafikia Wananchi.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wapya huku akiwaagiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao, kushuka hadi ngazi za chini na kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa kwa uharaka na ufanisi katika Awamu ya Pili ya Serikali ya Awamu ya Nane.


Hafla hiyo ya kuapishwa kwa viongozi hao ilifanyika leo Novemba 15, 2025 katika Viwanja vya Ikulu, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo Rais Mwinyi alieleza kuwa Serikali imejipanga kuweka mfumo maalum wa kutathmini utendaji wa kila wizara pamoja na watendaji wake ili kuongeza uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma.


Katika maboresho ya muundo wa Serikali, Dkt. Mwinyi alisema kuwa Serikali imeanzisha Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu ili kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za Serikali, hususan maeneo ya kifedha na ukusanyaji wa mapato. Aidha, aliweka bayana kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji yenye jukumu la kuendeleza na kuwawezesha vijana katika ajira na ujasiriamali.


Amesema kuwa baadhi ya wizara zilizokuwa chini ya Afisi ya Rais zimepunguzwa hadi tatu, huku mbili zikihamishiwa katika maeneo mengine ya Serikali lengo likiwa kuongeza ufanisi na kurahisisha usimamizi wa sekta hizo.


Rais Mwinyi aliwataka Mawaziri kuandaa mpango kazi unaofungamana na ahadi za kampeni, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, huku wakihakikisha wanatembelea miradi ya wizara zao ili kufuatilia thamani ya fedha, ubora wa ujenzi, kasi ya utekelezaji na kukamilika kwa wakati.


Katika eneo la matumizi ya fedha za umma, Dkt. Mwinyi alisisitiza nidhamu ya matumizi, akitaka upunguzaji wa safari za nje, udhibiti wa matumizi ya mafuta na kuimarisha uthibiti dhidi ya udanganyifu na ubadhirifu serikalini. Aliwataka pia kusimamia kwa karibu uwajibikaji wa watendaji walioko chini yao, kulinda mali za umma na kupambana na rushwa pamoja na uzembe.


Aidha, aliagiza kila wizara kuanzisha utaratibu wa kufanya tathmini za utekelezaji kila baada ya robo mwaka, na kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari ili wananchi waweze kufahamu hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto zao. Serikali, alisema, itaandaa mkataba maalum wa kupima utendaji wa viongozi na taasisi zilizo chini ya wizara husika.


Kuhusu upokeaji wa kero za wananchi, Rais Mwinyi alieleza kuwa Serikali itaweka mfumo maalum wa kusikiliza na kushughulikia changamoto hizo sambamba na mfumo wa Sema na Rais, ili kuongeza uwazi na ufanisi katika kujibu changamoto za wananchi.


Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Dkt. Mwinyi amelihimiza Chama cha ACT Wazalendo kutafakari upya umuhimu wa kurejea katika ushiriki wa Serikali hiyo kwa maslahi mapana ya Taifa, akibainisha kuwa Katiba bado inaendelea kutoa nafasi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kwa ushirikiano huo.






Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.