SERIKALI YAIPONGEZA FCC KWA KUIMARISHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI.


Na Fidea Masunga,Dar es salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), ameipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mazingira ya biashara na kulinda maslahi ya walaji nchini. 


Akizungumza wakati wa ziara yake katika ofisi za FCC jijini Dar es Salaam, Waziri Kapinga alisema tume hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kusimamia ushindani wa haki, hatua inayoongezea uchumi uthabiti na kuvutia wawekezaji.


Amesema Serikali inaendelea kuboresha sera na kupunguza urasimu ili kuunda mazingira rafiki zaidi kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wawekezaji. Waziri Kapinga alibainisha kuwa juhudi za FCC zimechangia kuimarisha sekta ya viwanda, kupanua wigo wa uzalishaji na kuongeza mauzo ya nje, hivyo kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa.


Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya viwanda na biashara ni muhimili muhimu katika uchumi wa Tanzania, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza ajira, kuchochea uzalishaji wa malighafi na kupanua maeneo ya uwekezaji ili kuongeza tija katika sekta hiyo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema tume inaendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa walaji, ikiwemo mpango wa kuanzisha Baraza la Kitaifa la Utetezi wa Walaji, ambalo linalenga kuongeza ushiriki wa wananchi na kuboresha ufuatiliaji wa mwenendo wa biashara nchini.


Bi. Ngasongwa ameongeza kuwa FCC itaendelea kufanya kazi kwa weledi na uwazi ili kuhakikisha ushindani wa biashara unazingatia haki, kanuni na maslahi ya walaji pamoja na wawekezaji.





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.