SERIKALI YAKEMEA TAARIFA POTOFU, YASEMA TANZANIA IKO SALAMA.
Serikali imesema imechukua hatua madhubuti kukabiliana na taarifa potofu zilizoenea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, na kusisitiza kuwa hali ya nchi iko shwari huku shughuli za kiuchumi zikiendelea kama kawaida.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameunda Tume Huru itakayochunguza kwa miezi mitatu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyosababisha vifo, majeraha na uharibifu wa mali.
Msigwa ameikosoa CNN, BBC, Al Jazeera na DW kwa kuripoti habari za upande mmoja, akisema wamekosa uadilifu wa kitaaluma kwa kupuuza taarifa sahihi kutoka Serikalini.
Aidha amevishukuru vyombo vya habari vya ndani kwa kuonesha uzalendo na kuipa kipaumbele maslahi ya Taifa.
Amesema pia kuna kampeni za kimtandao zinazoendeshwa kutoka nje ya nchi zenye lengo la kuichafua Tanzania, kuchochea chuki na kuathiri uchumi, na amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo.
Kwa upande wa watalii, Msigwa amesisitiza kuwa vivutio vyote vya utalii nchini ni salama na viko wazi, huku Serikali ikiendelea kusimamia kwa karibu hali ya usalama.
Msigwa amesema Tume ya Uchunguzi ikikamilisha kazi yake, Serikali itatoa taarifa rasmi kwa umma, na ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani na kuzingatia taarifa sahihi.

Comments
Post a Comment