SERIKALI YAZINDUA MIKAKATI YA KUWAPA FURSA VIJANA KATIKA UWEKEZAJI.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ametoa mikakati mipya ya kukuza uwekezaji nchini, ikilenga hasa kuwapa fursa vijana na kuongeza ajira.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Prof. Mkumbo alisema mikakati hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kusogeza uwekezaji karibu na wananchi.


“Tunataka uwekezaji unaowasaidia wananchi, hasa kuwapa fursa vijana,” alisema.


Serikali itazindua Kituo Maalumu cha Wawekezaji Vijana kinachotoa mafunzo na usaidizi kwa vijana, na pia kuwa na uwakilishi wa kitaifa. Vilevile, itazindua programu ya ardhi na viwanda kwa vijana waliomaliza vyuo, ili waweze kuwekeza katika maeneo maalumu kama Dodoma-Nala, Pwani-Kwala na Mara-Bunda.


Huduma za uwekezaji zitasogezwa hadi kila mkoa ifikapo mwaka 2028 kupitia vituo maalumu vya uwekezaji. Aidha, TISEZA itashirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya viwanda kwa gharama nafuu, huku pia kuanzishwa vivutio vipya vya uwekezaji na kuwashirikisha wawekezaji kutoa maoni ya kuboresha sheria.


Prof. Mkumbo alisema kuanzia Januari 2026, atakutana na wawekezaji kila miezi mitatu kujadili na kutathmini mwenendo wa uwekezaji. Eneo la kiuchumi la Bagamoyo pia litapewa kipaumbele kwa kuanzisha kongani ya viwanda inayolenga soko la ndani na nje, huku pia jitihada zikiendelea kuvutia uwekezaji katika kuzalisha bidhaa ambazo nchi inaagiza kwa wingi.


Mikakati hiyo inalenga kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha sekta binafsi, na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.