TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA HORTICULTURE: DKT. YONAZI AELEZA MAFANIKIO NA FURSA.


Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim James Yonazi, ameeleza mafanikio makubwa ya Tanzania katika sekta ya horticulture, akibainisha fursa za ukuaji, uwekezaji na ajira zinazotokana na kilimo cha kisasa cha mazao ya bustani.


Akizungumza katika uzinduzi wa Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Mazao ya Horticulture (HoBIS 2025) jijini Dar es salaam, Dkt. Yonazi, akimuwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kausiluka, alisema kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka tani milioni 1.1 mwaka 2003/04 hadi zaidi ya tani milioni 8.4 mwaka 2023/24, huku mauzo ya nje yakiongezeka kutoka dola milioni 64 hadi zaidi ya dola milioni 569.


“Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za wakulima, wajasiriamali, wasindikaji na wadau wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa,” alisema Dkt. Yonazi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).


Alibainisha kuwa Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, inaendelea kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na miundombinu, ikiwemo ujenzi wa maghala ya baridi, maboresho ya bandari na viwanja vya ndege. Alisisitiza kuwa horticulture inaweza kuwa injini ya mageuzi ya kiuchumi, ikichangia ajira, kipato na maendeleo ya kijamii kwa wananchi wengi.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi. Alionyesha kuwa kupitia ushirikiano huu, masoko zaidi ya tisa (9) yamefunguliwa, uwekezaji umeongezeka, na makampuni binafsi yameanzishwa kutoa ithibati za viwango, ikiwemo kampuni ya GREENCERT, tanzu ya TAHA, hatua inayolenga kuboresha ubora wa mazao ya kilimo nchini.


Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, aliwakaribisha wageni wote na kutoa hotuba ya ukaribisho. Pia alishukuru Serikali na Wizara ya Kilimo kwa ushirikiano unaosaidia sekta ya horticulture kukua na kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.


Mkutano huu umeunda jukwaa la wadau wa horticulture kutoka ndani na nje ya Afrika kushirikiana, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kukuza masoko mapya kwa mazao ya horticulture.





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.