Tanzania Yazindua Mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji Katika COP30 Brazil.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha Mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika jijini Belem, nchini Brazil.
Gridi ya Taifa ya Maji ni mkakati wa kitaifa unaotekelezwa chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, wenye lengo la kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma za maji kwa jamii, viwanda, kilimo, mifugo na mazingira, sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, amesema kuwa Gridi ya Taifa ya Maji itakuwa suluhisho muhimu katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji nchini.
Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwa kinara wa ajenda ya maji barani Afrika kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa binadamu.
Bw. Mitawi ameongeza kuwa utekelezaji wa gridi hiyo utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi na kuhakikisha huduma za maji zinakuwa za uhakika na endelevu.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mpango huo muhimu unafanyika kwa ufanisi na kukamilika kama ilivyopangwa.
Amesisitiza pia kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji vikiwemo maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika pamoja na mito mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa rasilimali maji unaendelea kudumu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.


Comments
Post a Comment