TCRA YAENDELEA KUHAMASISHA VILABU VYA KIDIJITI MASHULENI.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inashiriki kwenye Mkutano Mkuu wa Wenyeviti wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA) unaoendelea katika ukumbi wa Sephile Sapphire Pride Castle jijini Dodoma kuanzia Novemba 25 hadi 27, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, Meneja wa Masuala ya Wateja na Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano, Mhandisi Kadaya Baluhye, amesisitiza umuhimu wa kuanzisha vilabu vya kidijiti katika shule za msingi ili kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Amesema vilabu hivyo vitawajengea wanafunzi msingi wa matumizi sahihi na yenye tija ya TEHAMA wakiwa bado shuleni, hatua itakayowaandaa kuwa wabunifu na wataalamu wa teknolojia watakaoweza kuchangia kwa ufanisi kwenye uchumi wa kidijiti.
Ushiriki wa TCRA katika mkutano huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuhamasisha uanzishwaji wa vilabu vya kidijiti kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, kwa lengo la kuwaunganisha vijana katika jukwaa la majadiliano na majaribio ya TEHAMA kwa vitendo hatua ambayo inalenga kuzalisha kizazi cha wabunifu na wataalamu watakaotoa suluhisho za kiteknolojia nchini.


Comments
Post a Comment