TIRDO ,STAMICO WASAINI MKATABA WA UTAFITI WA MADINI YA KIMKAKATI NCHINI.

 


Morogoro.

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kushirikiana na Shirika la Madini Nchini (STAMICO) wamesaini makubaliano ya awali (MoU) kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini ya kimkakati katika mikoa ya Kagera na Singida.


Mkataba huo unalenga kuimarisha utafiti wa kitaalamu kuhusu madini muhimu kwa maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa, ukiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara katika kusukuma mbele ajenda ya mageuzi ya viwanda nchini.


Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Mtambo, alisisitiza umuhimu wa utafiti huo katika kuendeleza sekta ya viwanda na madini, akieleza kuwa utasaidia kubaini uwezo wa kiuchumi na viwandani wa madini ya kimkakati na kuweka msingi wa uendelezaji wake kwa tija zaidi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk. Venance Mwasse, alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta ya madini kwa kuunganisha nguvu za kitaalamu, utafiti wa kisayansi na ubunifu wa kiteknolojia.


Utafiti huo utaanza mara moja, ambapo kwa mkoa wa Singida utafanyika katika Wilaya ya Kiomboi, na kwa mkoa wa Kagera katika Wilaya ya Kyerwa.


Madini yatakayofanyiwa utafiti ni pamoja na Lithium, Cobalt, Nickel, Graphite, na Manganese, ambayo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, vifaa vya elektroniki na bidhaa za chuma cha pua.


Kupitia utafiti huu, TIRDO na STAMICO wanatarajia kupata takwimu sahihi zitakazowezesha Serikali kupanga kwa ufanisi mikakati ya uendelezaji wa madini hayo, kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi na kupunguza usafirishaji wa madini ghafi nje ya Tanzania.


Matokeo ya utafiti yatachangia kuandaa miradi ya kitaifa itakayowezesha upatikanaji wa fedha kutoka taasisi za kifedha, kuongeza ajira, kuboresha miundombinu na kuchochea ustawi wa jamii katika maeneo yatakayohusika.


Mbali na taasisi hizo mbili, wataalamu kutoka Shule ya Madini na Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nao watashiriki katika utafiti huo.


Hafla ya utiaji saini imefanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ujenzi, Morogoro, ambapo washiriki wameahidi kuanza kazi mara moja kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali zake kupitia utafiti wa kina wa kitaalamu.







Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.