ONGEZEKO LA JOTO KALI: TMA YATOA TAHADHARI KWA WANANCHI.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ongezeko la joto katika baadhi ya mikoa nchini, hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua hali ambayo imesababishwa na mwelekeo wa Jua la Utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo husika.
Kwa mujibu wa TMA, vipindi vya Jua la Utosi hufikia kilele mwishoni mwa Novemba pale jua linapokaribia Tropiki ya Kaprikoni na hujirudia Februari wakati jua linaelekea Tropiki ya Kansa. Ukaribu wa uso wa Dunia na miale ya jua husababisha ongezeko la joto, jambo linaloathiri hali ya anga na mwonekano wa hewa.
Katika mwezi Novemba 2025, ongezeko la joto limeendelea kujitokeza katika baadhi ya mikoa ambapo ripoti za vituo vya hali ya hewa zinaonyesha Moshi (Kilimanjaro) ilifikia 35.7°C mnamo 21 Novemba, ongezeko la 4.2°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu. Ilonga (Morogoro) iliripoti 35.5°C mnamo 20 Novemba, ongezeko la 2.7°C, Morogoro 34.5°C mnamo 26 Novemba (ongezeko la 2.3°C), Ibadakuli (Shinyanga) 33.6°C mnamo 14 Novemba (ongezeko la 2.2°C) na Dar es Salaam 33.2°C mnamo 19 na 21 Novemba (ongezeko la 1.6°C).
TMA pia imebainisha kwamba ongezeko la unyevu angani, hususan katika ukanda wa pwani na maeneo jirani, limechangia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vilivyoripotiwa.
Aidha, vipindi vya mvua vinatarajiwa kuanza mwezi Desemba 2025, jambo linalosababisha kupungua kwa joto katika baadhi ya mikoa.
Hata hivyo TMA imewashauri Wananchi kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.



Comments
Post a Comment