TTCL Yazindua T-Fiber Triple Hub, Kifurushi cha Huduma Tatu kwa Gharama Nafuu.
Na Fidea Masunga,Dar es Salaam.
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua kifurushi kipya cha mawasiliano kinachoitwa T-Fiber Triple Hub, chenye lengo la kumrahisishia mteja kupata huduma tatu muhimu kwa gharama nafuu.
Kifurushi hicho, ambacho kinatajwa kuwa cha kwanza nchini, kinajumuisha huduma ya intaneti ya kasi bila kikomo, simu ya mezani, na huduma ya intaneti na dakika kwa simu ya mkononi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uhusiano na Uendelezaji wa Bidhaa wa TTCL, Bi. Janeth Maeda, alisema kifurushi hicho ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano na kuongeza ufanisi kwa wateja.
“Kupitia T-Fiber Triple Hub, tunalenga kumpunguzia mteja usumbufu kwa kumpatia huduma zote tatu kupitia kifurushi kimoja kwa gharama nafuu,” alisema Bi. Maeda.
Kwa gharama ya kuanzia Sh70,000 kwa mwezi, mteja wa T-Fiber Triple Hub atapata intaneti yenye kasi hadi 20 Mbps, dakika 300 za mawasiliano, pamoja na GB 20 kwa matumizi ya simu ya mkononi.
Bi. Maeda alisema kifurushi hicho kinawawezesha wateja kutumia dakika na data hizo popote walipo, nyumbani au kazini, jambo linaloongeza urahisi na ufanisi katika mawasiliano.
“Tunawaalika Watanzania wote kujiunga nasi katika hatua hii mpya ya ubora, urahisi na thamani kupitia T-Fiber Triple Hub,” aliongeza.




Comments
Post a Comment