UVCCM yatoa tamko la kulaani vurugu za Oktoba 29–30, 2025.
Yawataka vijana kudumisha amani na uzalendo wa Taifa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umetangaza rasmi kulaani kwa nguvu zote vurugu na fujo zilizojitokeza nchini tarehe 29 na 30 Oktoba 2025, ukivitaja vitendo hivyo kama kinyume cha sheria, maadili ya kijamii na misingi ya amani ya Taifa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya UVCCM, Upanga – Dar es Salaam, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohammed Ali Kawaida (MCC), alisema vurugu hizo ziliacha majeraha ya kijamii, hasara za kiuchumi na doa katika sura ya umoja wa Watanzania.
“Nina huzuni kubwa kuona vijana wetu, ambao ni nguvu kazi ya Taifa, wamehusika katika matendo ya fujo na vurugu. Hii si tu kinyume cha sheria, bali ni kinyume cha uzalendo na maadili ya Mtanzania,” alisema Kawaida kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa ni jukumu la vijana kuhakikisha amani ya Tanzania inaendelea kudumu, kwani amani ndiyo msingi wa maendeleo na mafanikio ya Taifa.
“Ninakemea na kulaani kwa dhati vitendo hivi. Vijana tunapaswa kuwa walinzi wa amani, si vyanzo vya machafuko. Amani yetu ni urithi kutoka kwa waasisi wa Taifa letu, tusiiweke rehani kwa misukumo ya kisiasa,” alisisitiza.
Aidha, aliwaonya watu wanaoishi ndani na nje ya nchi wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu, akisema Serikali na taasisi za vijana zitaendelea kufuatilia mienendo hiyo kwa karibu.
Kawaida alisema UVCCM itaendeleza mikakati ya kuwaelimisha vijana kuhusu uzalendo, maadili na umuhimu wa kulinda amani kama urithi wa Taifa, akisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha utulivu barani Afrika.

Comments
Post a Comment