VETA NA PPRA WATIA SAINI MAKUBALIANO YA KUSHIRIKIANA KUWEZESHA MAKUNDI MAALUM KUNUFAIKA NA ZABUNI ZA UMMA.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), leo tarehe 20 Novemba 2025, wametiliana saini makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha makundi maalum nchini kunufaika zaidi na fursa za zabuni katika taasisi za ummaMakubaliano hayo yametiwa saini jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya PPRA.
Makundi maalum yanayolengwa ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2023, taasisi za umma zinapaswa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.
Akizungumza kabla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema PPRA inaishukuru VETA kwa kukubali kushirikiana katika kuhakikisha makundi maalum yanapata nafasi stahiki kwenye mnyororo wa ununuzi wa umma kama inavyoelekezwa na sheria.
“Sheria inaelekeza asilimia 30 ya ununuzi wa umma itolewe kwa makundi maalum. Ni jukumu letu kama taasisi kuhakikisha tunawafikia vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu,” amesema Simba.
Pamoja na fursa hizo, Simba amesema changamoto iliyopo ni kwamba makundi hayo bado hayajafaidika ipasavyo, kwani hadi sasa ni makundi 1,000 tu yaliyopata mikataba yenye thamani ya Shilingi Bilioni 30.
“Tukitekeleza vyema, tunaweza kufikia mikataba ya thamani ya trilioni 5. PPRA tumejipa lengo la kufikia makundi 20,000,” ameongeza.
Simba amesema ushirikiano na VETA ni muhimu kwa kuwa taasisi hiyo ina uzoefu mkubwa wa kufanya kazi na makundi maalum kupitia kuwapatia ujuzi na kuwajengea uwezo.
Amefafanua kuwa ushirikiano huo utasaidia kufundisha, kusajili na kuwaandaa wanufaika kushiriki kikamilifu katika zabuni mbalimbali.
Aidha, amesema PPRA itashirikiana na VETA kusaidia hata wahitimu wapya wenye nia ya kufanya kazi na Serikali kwa kulegeza baadhi ya vigezo vinavyoweza kuwazuia kupata zabuni.


Comments
Post a Comment