WAKAZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM WAENDELEA KUMIMINIKA KATIKA KAMBI YA UCHUNGUZI NA MATIBABU BILA MALIPO INAYOTOLEWA NA HOSPITALI YA AMANA NA GSM FOUNDATION.


Mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani wameendelea kujitokeza kwa wingi katika kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi inayoendeshwa bila malipo na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana kwa ushirikiano na GSM Foundation. Hii ni siku ya pili mfululizo tangu kuzinduliwa kwa huduma hizo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.


Wananchi wameonekana kuthamini kwa kiasi kikubwa uwepo wa kambi hiyo, ambayo imekuwa mkombozi kwa watu wa kada mbalimbali, hususan wale wasioweza kumudu gharama za huduma za kibingwa. 


Huduma zinazotolewa zimegusa maeneo muhimu ya afya ikiwemo uchunguzi na matibabu ya macho, afya ya kinywa na meno, magonjwa ya akina mama na afya ya uzazi, magonjwa ya ngozi, uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, matumizi sahihi ya dawa, huduma kwa watoto, pamoja na magonjwa ya masikio, pua na koo.


Aidha, kambi hii imekuwa fursa muhimu kwa wananchi kupata elimu ya afya, ikiwemo namna ya kujikinga dhidi ya magonjwa sugu na kuishi kwa kuzingatia kanuni za lishe bora. Wengi wameeleza kufarijika na huduma za kitaalamu wanazopata pamoja na upatikanaji wa vipimo ambavyo kwa kawaida vinahitaji gharama kubwa.


Kambi hiyo ilianza rasmi tarehe 28 Novemba na itahitimishwa tarehe 30 Novemba 2025. Sambamba na utoaji wa huduma za matibabu, GSM Foundation kwa kushirikiana na Hospitali ya Amana pia inatoa bima za afya bila malipo kwa makundi maalum ambayo ni Wanawake, Wazee na Watoto wasio na uwezo, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.