Waziri Kapinga Aipongeza TIRDO kwa Kuchochea Maendeleo ya Viwanda.


Na Fidea Masunga,Dar es salaam.

 Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amelipongeza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa mchango wake mkubwa katika kukuza sekta ya viwanda na teknolojia nchini.


Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika shirika laTIRDO jijini Dar es salaam, Waziri Kapinga alitembelea maabara mbalimbali na kukutana na vijana wabunifu wanaosaidiwa na shirika hilo, wakiwemo wanaotengeneza magari ya umeme (KAYPEE Motors), wanaochakata plastiki (PREYO), na wabunifu wa vifaa vya kielektroniki (HOP).


Waziri Kapinga alisema Serikali itaendelea kuisaidia TIRDO kufanya tafiti bunifu zitakazoongeza ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa viwanda. 


Alibainisha kuwa ushirikiano huo utaiwezesha TIRDO kubuni vyanzo vipya vya mapato, kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kuboresha mazingira ya biashara, na kuleta maendeleo endelevu.


Aidha, Waziri Kapinga alibainisha kuwa mapato ya makaa ya mawe yaliyotokana na tafiti na maabara za TIRDO yameongezeka kutoka shilingi bilioni 20 hadi bilioni 90, jambo lililookoa fedha za kuepuka uagizaji kutoka nje, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, na kuchochea ukuaji wa teknolojia ya ndani.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Mtambo, alisema shirika limejipanga kuanzisha kituo maalumu cha kutengeneza vifaa vya kielektroniki ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kukuza viwanda vya ndani. 


Prof. Mtambo pia alibainisha mafanikio ya shirika ikiwemo utafiti wa Mradi wa Magadi Soda Engaruka, ujenzi wa kiwanda cha kukoboa mpunga Mkuyuni Mwanza, na ukaguzi wa viwanda zaidi ya 50, ambapo viwanda 22 vilirejeshwa serikalini.






Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.