ACP. MLAWA AWATAKA MAAFISA NA ASKARI KUONGEZA KASI YA UZALISHAJI CHAKULA.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Matilda Mlawa, leo Disemba 15, 2025, amefanya ziara ya ukaguzi wa maandalizi ya kilimo cha mpunga kwa msimu ujao katika shamba la kimkakati la vituo vya Magereza ya mkoa Lindi, lenye ukubwa wa ekari 100, lililopo katika Kambi ya Kilimo Makangaga, inayosimamiwa na Gereza la Kingurungundwa.
Ziara hiyo ya ukaguzi imelenga kutekeleza agizo la Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, linalotaka kila mkoa wa Magereza nchini kujitosheleza kwa uzalishaji wa chakula kwa ajili ya kuwalisha wafungwa na mahabusu waliopo katika vituo vyao.
Katika ukaguzi huo, ACP Mlawa alikagua miundombinu mbalimbali ya kilimo ikiwemo nyenzo za kilimo, maandalizi ya mashamba pamoja na mipango ya uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi, kasi na ushirikiano ili kuhakikisha mavuno ya kutosha yanapatikana kwa wingi msimu ujao.
Aidha, ACP Mlawa alitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Utawala la Gereza la Kingurungundwa, ambapo aliwapongeza Maafisa na askari kwa hatua iliyofikiwa, huku akiwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Kingurungundwa, Mrakibu wa Magereza (SP) Geoffrey Mgallah, ameahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maagizo na mikakati yote iliyopangwa kwa ajili ya msimu wa kilimo, na kusisitiza kuwa kambi hiyo ipo chini ya usimamizi wake wa moja kwa moja, pamoja na kuahidi kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la utawala ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliokusudiwa.



Comments
Post a Comment