BONDIA MWAKINYO KUIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA KESHO KATIKA PAMABANO LA KIMATAIFA DHIDI YA MNAIJERIA STANLEY ERIBO.
Bondia wa kimataifa Hassan Mwakinyo ataipeperusha bendera ya Tanzania dhidi ya mpinzani wake kutoka Nigeria, Stanley Eribo, katika pambano la Boxing on Boxing Day litakalofanyika kesho, Desemba 26, 2025, kwenye Ukumbi wa Warehouse, Masaki jijini Dar es Salaam.
Mwakinyo, ambaye ameongoza mabondia wengine leo kupima uzito, amesema yuko tayari kikamilifu kwa pambano hilo, akiahidi ushindi kwa Watanzania.
Akizungumza mara baada ya zoezi la upimaji uzito, Mwakinyo alisema, “Nimejiandaa vizuri sana kwa pambano hili. Nimemuandaa mpinzani wangu kikamilifu na nawahakikishia Watanzania ushindi mkubwa. Nitaingia ulingoni kuipigania heshima ya taifa.”
Kwa upande wake, bondia wa Tanzania Hamadi Furahisha alisema maandalizi yake yamekamilika na yuko tayari kukabiliana na mpinzani wake kutoka Malawi, Hanock Phiri.
“Najua ninampinzani mkali, lakini niko tayari kumpa pambano gumu na kuwaburudisha mashabiki,” alisema Furahisha.
Naye bondia kutoka Nigeria, Stanley Eribo, alisema amekuja Tanzania kwa lengo la ushindi, akisisitiza kuwa heshima ipo lakini ulingoni ni mapambano.
“Nimekuja Tanzania kwa ajili ya ushindi. Heshima ipo, lakini ulingoni nitapambana kwa nguvu zangu zote,” alisema Eribo.
Kwa upande wa wanawake, bondia Debora Mwenda alisema yuko tayari kuwakilisha vyema wanawake wa Tanzania katika pambano lake dhidi ya bondia kutoka Malawi, Mariam Dick.
“Nimefanya maandalizi ya kutosha. Natambua ukubwa wa pambano, lakini niko tayari kuwakilisha wanawake wa Tanzania kwa ushindi,” alisema Debora.
Mratibu wa Matukio kutoka Peak Time, Bakari Hatibu, alisema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika kwa asilimia 90, huku mabondia wote wakiwa tayari kuingia ulingoni.
“Mabondia wote wamewasili salama na maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa. Kilichobaki ni mashabiki kujitokeza kushuhudia burudani kubwa ya kufunga mwaka,” alisema Hatibu.
Katika mapambano mengine, Ally Ngwando atachuana na Mussa Makuka, huku mapambano hayo yote yakitarajiwa kutoa burudani kubwa kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi.




Comments
Post a Comment