DKT. MWIGULU NCHEMBA ATOA WITO KUDUMISHA AMANI, AWAHIMIZA VIONGOZI WA DINI KUPINGA MIGAWANYIKO.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya umoja na amani, kupinga chuki, migawanyiko na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga mshikamano wa Taifa.
Amesema vita au migogoro inayohusisha wananchi wa taifa moja haina mshindi, bali husababisha hasara kwa wote na kuacha majeraha ya kudumu katika jamii. Aidha, mgawanyiko wa kitaifa huathiri maendeleo na ustawi wa nchi kwa ujumla.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo leo, Alhamisi Desemba 25, 2026, aliposhiriki Ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri la Azania Front jijini Dar es Salaam.
“Manufaa ya amani ni makubwa. Amani huleta maendeleo ya kiuchumi, huimarisha ustawi wa jamii na huwezesha kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa,” amesema.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa nchi, huku ikiendelea kuwajengea Watanzania, hususan vijana, misingi ya uzalendo, maadili mema na kuthamini umoja wa kitaifa.
“Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha umoja, amani, mshikamano na utulivu katika ukanda wetu na barani Afrika. Amani hii imejengwa juu ya misingi imara ya maadili, haki, kuheshimiana, uvumilivu na uzalendo,” amesema.
Aidha, katika ibada hiyo, Dkt. Nchemba ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwatakia Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla heri ya Sikukuu ya Krismasi, huku akiwahimiza kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani, upendo na utulivu, na kuendelea kudumisha mshikamano wa kitaifa kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Askofu Dkt. Alex Malasusa, amekemea tabia za baadhi ya watu za kuchafua taswira za watu wengine na kuichonganisha jamii.
Askofu Malasusa amesema kuna watu ambao hawapati furaha wanapoona jamii ikiishi pamoja kwa amani, akisisitiza umuhimu wa kulinda umoja, mshikamano na maadili ya Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



Comments
Post a Comment