FCC YAPOKEA TUZO MAALUM KWA MCHANGO WAKE KATIKA KUIMARISHA SEKTA YA MANUNUZI NA UGAVI.



TUME ya Ushindani (FCC) imetunukiwa tuzo maalum ya kutambua mchango wake katika maendeleo na uimarishaji wa Sekta ya Manunuzi na Ugavi nchini, ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi zake katika kulinda na kusimamia ushindani wa haki, uwazi na ufanisi ndani ya sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mshamu Munde, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, na kupokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha FCC, Bi. Roberta Feruzi, katika hafla rasmi ya utoaji wa tuzo iliyofanyika jijini Arusha.


Hafla hiyo iliambatana na Kongamano la 16 la Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), na kuandaliwa na Bodi ya Wataalamu na Mafundi wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), likiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya manunuzi na ugavi kutoka ndani na nje ya nchi.


Katika kongamano hilo, FCC ilishiriki kama mdau muhimu wa sekta ya manunuzi na ugavi, ambapo iliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuzingatia ushindani wa haki katika masuala ya manunuzi na ugavi, hususan katika kulinda na kuimarisha mnororo wa thamani kwa manufaa ya wadau wote.


Aidha, kupitia kongamano hilo, Tume ilitoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu majukumu na kazi zake, ikisisitiza nafasi yake katika kuhakikisha mazingira ya ushindani yanayochochea uwazi, ufanisi na maendeleo endelevu ya sekta ya manunuzi na ugavi nchini.


FCC imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kuimarisha mifumo ya ushindani wa haki, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuchangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla.





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.