SERIKALI YAIPONGEZA FCC KWA KUIMARISHA USHINDANI WA HAKI NA ULINZI WA WALAJI.


Na Fidea Masunga.


Serikali imeipongeza Tume ya Ushindani (FCC) kwa kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria za ushindani na ulinzi wa walaji, hatua inayosaidia kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani kuelekea Dira ya Taifa ya 2050. 


Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Patrobas Katambi,katika kongamano la kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Judith Kapinga, Katambi alisema kuwa kulinda mlaji katika matumizi ya Akili Mnemba (AI) ni nguzo muhimu katika usalama wa uchumi wa taifa kwani matumizi ya AI yanahitaji kuendana na ulinzi wa watumiaji na ushindani wa haki, ili kuhakikisha masoko yanabaki salama, wazi na yenye usawa kwa wote.


Katambi alibainisha kuwa Serikali katika kipindi cha pili cha Awamu ya Sita imejipanga kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara, kuwezesha wafanyabiashara kupata faida halali na kuchangia kikamilifu katika ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa. 


“Serikali imejipanga kuwa daraja, si ukuta, katika kuhakikisha sera za TEHAMA na AI zinazolinda walaji na wafanyabiashara zinatekelezwa kikamilifu,” alisisitiza.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho hayo yalianza rasmi Disemba 01,2025 yakitanguliwa na mkutano na vyombo vya habari, semina kwa mamlaka za udhibiti, mafunzo kwa wanasheria na kampeni za elimu kwa wananchi, ikiwa ni njia ya kuongeza uelewa kuhusu sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.


Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT), Jaji Rose Ebrahim, aliwataka wananchi na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za vitendo vya ukiukwaji wa haki kama vile bidhaa feki na ubabaishaji wa bei, ili kulinda ustawi wa uchumi na maslahi ya walaji.


Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani, Dkt. Aggrey Mlimuka, alisema FCC imejipanga kuendeleza usimamizi madhubuti wa masoko, kupunguza mianya ya upotoshaji wa ushindani, kulinda mlaji na kudhibiti matumizi mabaya ya AI katika biashara. Alisema AI ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uwazi, uadilifu na ufanisi katika masoko.


Siku ya ushindani duniani huadhimishwa Disemba 05 kila mwaka ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Akili Mnemba (AI) katika Kudumisha Ushindani wa Haki na Kulinda Walaji,” ikionyesha umuhimu wa AI katika kuongeza uwazi, ufanisi na ushindani katika masoko.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.