FCC YASISITIZA UMUHIMU WA AKILI MNEMBA (AI) KATIKA KUDUMISHA USHINDANI WA HAKI TANZANIA.


Tume ya Ushindani (FCC) imeendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha ushindani wa haki katika soko la Tanzania, huku ikitambua mchango mkubwa wa teknolojia za kisasa, hususan Akili Mnemba (AI), katika kuboresha biashara, huduma, na faida kwa walaji.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani 2025, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bi. Khadija Ngasongwa amesema AI ina nafasi muhimu katika kukuza ubunifu endelevu, kuongeza tija, na kuhakikisha ushindani wa haki kati ya makampuni yanayotoa bidhaa na huduma nchini.


“Tumetambua kwamba teknolojia na mfumo wa TEHAMA, ikiwa ni pamoja na Akili Mnemba, ni nyenzo muhimu katika kudhibiti ushindani wa kibiashara. Matumizi sahihi ya teknolojia hizi yanachangia kupunguza gharama za uendeshaji, kuboresha huduma, na kufungua fursa mpya za masoko,” amesema Bi. Ngasongwa.


Aidha Bi. Ngasongwa amesema kwamba katika juhudi zake za kudhibiti makubaliano ya kibiashara yanayofifisha ushindani, matumizi mabaya ya nguvu ya soko, na miungano ya makampuni inayoweza kuathiri ushindani, teknolojia za kisasa zinaweza kuwa msaada mkubwa wa kielektroniki katika ufuatiliaji na upelelezi wa masuala haya.


Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani hapa nchini mwaka huu yanafanyika kuanzia Disemba 1 hadi Disemba 5, 2025, na kilele chake kitaambatana na Kongamano Maalum la Ushindani litakalofanyika kwenye Hotel ya King Jada, Morocco Square, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi wa kongamano hilo atakuwa Mhe. Judith Salvio Kapinga, Waziri wa Viwanda na Biashara.


Kauli mbiu ya mwaka huu, “Artificial Intelligence (AI), Consumers and Competition Policy” au kwa Kiswahili, “Akili Mnemba (AI), Walaji na Sera za Ushindani”, inalenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa AI katika kuimarisha ushindani, kupanua fursa kwa wajasiriamali, na kuboresha huduma kwa walaji nchini.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.