MAAFISA USAFIRISHAJI WAHIMIZWA KUSHIRIKI MAFUNZO YA UDEREVA ILI KUWA MAHIRI.
Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataka maafisa usafirishaji, hasa bodaboda, kuhudhuria mafunzo ya udereva yanayolenga kujenga uelewa wa sheria, alama, na michoro ya usalama barabarani.
Kauli hiyo ilitolewa wakati akifungua mafunzo ya muda mfupi kwa zaidi ya vijana 200 wa Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe, waliyojiandikisha kushiriki mafunzo hayo yanayotolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi – VETA.
Akielezea umuhimu wa mafunzo hayo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa, alisema:
“Mafunzo haya yanalenga kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na uzembe na kutokujua sheria, kanuni, na taratibu za usalama barabarani kwa maafisa usafirishaji.”
Aidha, Mwenyekiti wa Vijana Kata ya Kiwira, ndugu Furaha Mwakyusa, aliwahimiza vijana kuendelea kujisajili kushiriki mafunzo hayo ili kuwa mahiri katika udereva na kupata cheti na leseni ya udereva, ambayo itathibitisha uhalali wao wa kuendesha vyombo vya moto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo cha VETA, Mhandisi Rajabu Ghuliku, alisema:
“Tunaendelea kuratibu na kuendesha mafunzo mbalimbali kwa makundi tofauti, ikiwemo madereva, ili kujenga uelewa, umahiri na weledi katika usalama barabarani.”
Mafunzo hayo yanafadhiliwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Mhe Patrick Mwalunenge, kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa usafirishaji kuhusu sheria, kanuni, taratibu, alama na michoro ya usalama barabarani, ili kuepuka ajali na kuongeza ulinzi wa maisha barabarani.
Mafunzo haya yanahusisha nyenzo za kitaaluma, mazoezi ya vitendo, na mitihani ya kutathmini umahiri wa washiriki, jambo linalolenga kuboresha usalama barabarani na weledi wa maafisa usafirishaji katika mkoa wa Mbeya.

Comments
Post a Comment