MAANDAMANO YA DISEMBA 09 NI HARAMU, SIMBACHAWENE ASEMA YATADHIBITIWA KWA MUJIBU WA SHERIA.
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Boniface Simbachawene, amesisitiza kuwa maandamano yanayohamasishwa kufanyika kesho, Jumanne Desemba 9, 2025, ni haramu kwa kuwa hayakufuata taratibu, sheria na miongozo inayosimamia mikusanyiko ya umma nchini.
Ametoa onyo hilo leo, Jumatatu Desemba 8, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Akifafanua msimamo wa Serikali, Mhe. Simbachawene alisema maandamano yanayodaiwa kuwa ya “amani” hayajaeleza waandaaji, mahali yatakapofanyika, wala mwelekeo wake vigezo ambavyo ni sharti la kisheria kwa maandamano yoyote yanayoruhusiwa na Katiba na sheria za nchi.
Alibainisha kuwa taarifa zilizopo zinaeleza kuwa maandamano hayo hayana ukomo na yanatarajiwa kuwa makubwa kuliko ya Oktoba 29, ambayo yalisababisha vifo, uharibifu wa mali, na kuyumbisha hali ya usalama.
“Maandamano mengine ya Oktoba 29 yalileta madhara makubwa vifo, uharibifu wa vituo vya mafuta, majengo ya Serikali na hata vituo vya polisi. Sasa tunapoambiwa haya ya Desemba 9 yatakuwa makubwa kuliko yale, hayo si maandamano; hayo ni ishara za mapinduzi,” alisema Simbachawene.
Waziri alikumbusha kuwa, kwa mujibu wa sheria, maandamano yanapaswa kuombwa na mtu au kikundi maalum, yawe na ujumbe ulio wazi, yaainishe muda na njia yatakazotumia, ili Jeshi la Polisi liweze kutoa ulinzi na kusimamia usalama wa washiriki na mali za wananchi. Alisema kutokuwepo kwa taarifa hizi kunathibitisha kuwa tukio hilo halina uhalali wa kisheria.
Aidha, Mhe. Simbachawene aliwahimiza wananchi kutokujihusisha, kushabikia, au kufuatilia maandamano hayo, ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa hatua hiyo si tu inahatarisha usalama, bali pia inapingana na sheria za nchi. Aliongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viko tayari kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha amani inaendelea kudumu.
Waziri pia aliwashukuru viongozi wa dini kwa mchango wao katika kuhamasisha utulivu na kudumisha umoja wa Taifa kufuatia sintofahamu iliyojitokeza baada ya matukio ya Oktoba 29, akisema juhudi hizo zimechangia kurejesha hali ya utulivu nchini.
Akihitimisha, Mhe. Simbachawene alitoa rai kwa wote “walioichoka amani” kuheshimu misingi ya sheria na utaratibu wa nchi, akibainisha kuwa Serikali haitasita kuweka nguvu zake kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa bila kusita.

Comments
Post a Comment