MECIRA YATOA ONYO KWA KENYA NA MAREKANI KUHUSU AMANI YA TANZANIA.


Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) kimeyataka mataifa ya Kenya na Marekani kuheshimu uhuru wa ndani wa Tanzania, mamlaka yake ya kikatiba na mshikamano wa kijamii wa Watanzania.


Kituo hicho pia kimeonya dhidi ya kuhalalisha au kuunga mkono uhamasishaji wa vurugu kwa kisingizio cha haki za binadamu au uhuru wa kujieleza, hususan kupitia taarifa zisizothibitishwa na zinazochochea chuki za kidini, kikabila au kisiasa.


Mwenyekiti wa MECIRA, Habibu Mchange, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, kufuatia hatua zilizochukuliwa na kituo hicho kuziarifu Serikali za Marekani na Kenya kuhusu taarifa potofu dhidi ya Tanzania pamoja na uhamasishaji wa vurugu na machafuko yaliyotokea Oktoba 29, 2025.


“Katika barua yetu kwa Ubalozi wa Marekani, tumeweka bayana kuwa tunalitambua na kuliheshimu taifa la Marekani linalojengwa juu ya misingi ya demokrasia, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza,” alisema Mchange.


Alisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza una mipaka yake ya kisheria na haupaswi kutumika kuhamasisha vurugu au vitendo vinavyohatarisha maisha ya watu katika nchi nyingine.


Mchange alisema hakuna mtu anayepaswa kutumia nchi ya kigeni kama kimbilio au jukwaa la kupanga na kuhamasisha vurugu dhidi ya nchi yake, na aliwahi kuongeza kuwa wahusika wote wa machafuko yaliyosababisha vifo wanapaswa kuwajibishwa kisheria bila kujali wanapopatikana.


“Kanuni hii imethibitishwa kimataifa pale ambapo wahamasishaji wa mauaji ya kimbari na machafuko makubwa katika nchi mbalimbali walichukuliwa hatua za kisheria kwa misingi ya uwajibikaji binafsi wa jinai,” alisema Mchange.


Aidha, aliomba ushirikiano wa kidiplomasia na kisheria kutoka Serikali ya Marekani, ikiwemo kurejeshwa kwa Mange Kimambi ili ajibu madai yanayomkabili kwa mujibu wa sheria.


Mchange aliongeza kuwa baadhi ya Watanzania wanaohamasisha machafuko wamekimbilia au wanaishi nchini Kenya, ambako wanapanga, kuratibu na kusambaza ujumbe unaohatarisha amani ya Tanzania kupitia mitandao ya kijamii.


“Tumetaja majina ya Hilda Newton, Twaha Mwaipaya na Edgar Sativa kuwa wanashiriki kikamilifu katika kampeni hizi kwa kushirikiana na Mange Kimambi,” alisema.


Alieleza wasiwasi wake kuhusu matamshi ya hadharani yanayodokeza baadhi ya raia wa Kenya kuunga mkono ajenda hizo, akisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza haujumuishi haki ya kuhamasisha vurugu au kusababisha vifo.


“Kwa mujibu wa sheria za kimataifa na za kikanda, uhamasishaji unaosababisha kupotea kwa maisha ya watu ni uhalifu mkubwa unaobeba uwajibikaji binafsi wa jinai,” aliongeza.


MECIRA ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuheshimu uhuru wa ndani wa Tanzania, kutumia taarifa zilizothibitishwa na zenye mizania, na kuepuka ujumbe unaopandikiza chuki za kidini, kikabila au kisiasa.


Vilevile, aliwahimiza Watanzania kuendelea kulinda amani, mshikamano wa kitaifa na maelewano ya kidini ili kuepuka kushawishiwa kujiingiza katika mipango ya vurugu au machafuko.


Aliwataka vyombo vya habari, wanaharakati na viongozi wa kijamii kutumia uhuru wao kwa uwajibikaji, wakitambua kuwa maneno na ujumbe wanaoutoa vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.


“Vijana watambue kuwa kushiriki katika uhamasishaji wa machafuko kunaweza kuwasababishia madhara makubwa ya kisheria, kijamii na kifamilia,” alionya.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.