NAIBU WAZIRI KATAMBI AIPONGEZA TIRDO, AAGIZA KUFUFUA VIWANDA VILIVYOKUFA.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi, ameliagiza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kuchunguza viwanda vilivyokufa na kutoa ushauri wa kitaalamu ili viweze kurejea kwenye uzalishaji, kutoa ajira, na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika TIRDO Desemba 22, 2025, Katambi alisema kero kubwa kwa wananchi ni kuona viwanda vipo lakini havifanyi kazi, ilhali vinaweza kutoa ajira na kusaidia uchumi wa nchi.
Aidha, Mhe. Katambi aliipongeza TIRDO kwa jitihada zake za kusaidia sekta ya viwanda nchini kupitia tafiti za teknolojia zinazofaa na kusambaza matokeo kwa wadau wa ndani na nje ya nchi. Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuendelezwa ili kufanikisha matokeo chanya na kujenga uhimilivu wa viwanda.
Naibu Waziri pia aliitaka TIRDO kutoa ushauri wa kitaalamu unaozingatia viwango vya sayansi na teknolojia, kusaidia viwanda kuwa na uhimilivu na kurahisisha ushindani katika masoko. Aliongeza kuwa utafiti unapaswa kuzingatia thamani ya fedha, uwekezaji wa viwanda, miundombinu, na kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Kushindana ni lazima tufanye tafiti tukitambua wapo wengine wanaoshindana nasi. Tutambue vikwazo, tujifunze kwa waliofanikiwa, tutambue mipaka yetu, na tuwe taifa makini lenye mapinduzi ya viwanda,” alisema Katambi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi (DED) wa TIRDO, Ramsons Mwilangali, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Prof. Mkumbukwa Mtambo, alisema shirika linaendelea kusaidia sekta ya viwanda nchini kwa kufanya tafiti za teknolojia zinazofaa, kusimamia na kusambaza matokeo ya tafiti kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.



Comments
Post a Comment