RAIS SAMIA ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 1,036, 1,014 WAPUNGUZIWA ADHABU KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 64 YA UHURU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametangaza msamaha kwa wafungwa 1036 katika kuadhimisha Miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Aidha, wafungwa wengine 1014 wamepunguziwa adhabu zao baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa kisheria.
Msamaha huo umetolewa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Rais chini ya Ibara ya 45(1)(a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo taarifa ya msamaha huo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. George Simbachawene, ambaye ameeleza kuwa utekelezaji wake unaanza mara moja katika vituo vyote vya magereza nchini.
Amesema kuwa msamaha huo hauwahusu wafungwa waliohukumiwa kwa makosa makubwa na hatarishi kwa jamii yakiwemo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, rushwa, biashara ya dawa za kulevya, makosa ya kujamiana, utekaji na wizi wa watoto, kuwapa mimba wanafunzi, pamoja na biashara haramu ya binadamu.
Pia hauwahusu wenye makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu au silaha, umiliki haramu wa silaha, kukutwa na viungo vya binadamu, ujangili na nyara za Serikali, wizi au ubadhilifu wa mali ya umma, ugaidi, uharamia, na makosa ya kimtandao ambapo hata Wafungwa waliokutwa na hatia ya mauaji pia hawajumuishwi kwenye msamaha huo.
Wengine ambao hawatanufaika na msamaha wa mwaka huu ni wafungwa wa maisha, waliokatiwa adhabu ya kifo, pamoja na wale ambao tayari wameshawahi kupata msamaha wa Rais katika miaka iliyopita.

Comments
Post a Comment